Tuesday, February 23, 2016


Monday, February 22, 2016

TCRA Yaifungia Video mpya ya Wimbo ‘Zigo remix’ ya AY Aliyomshirikisha Diamond Platnumz



Ambwene Yessaya ‘AY’ amethibitisha kupokea taarifa ya kufungiwa kwa video ya wimbo ‘ Zigo remix’ aliyomshirikisha Diamond Platnumz.

Akizungumza na 225 katika kipindi cha XXL cha Clouds FM, Jumatatu hii, AY amesema alipokea barua yenye amri hiyo kutoka kwa rafiki yake ambae anafanya kazi katika chombo kimoja cha habari.

“Sijaelewa maadili gani kwa sababu kama maadili niliyokosea mimi ni kushoot kwenye swimming pool, na kama kwenye swimmig pool watu nimevalisha jeans au maturubai hapo nitakuwa nimekosa maadili,” alisema AY.

“Mavazi ya kwenye swimming pool yako kila mahali, hata kwenye taarifa za habari (Michezo) wanaonyesha waogeleaji, kama hiyo pia ni kukiuka maadili ni sawa. Inashangaza mamlaka zetu wanafocus kwenye kufungia nyimbo zetu na kuacha video za nje. Sijawahi sikia muziki wa Kenya, Uganda au Marekani umefungiwa, kama wanaona nyimbo za Nicki Minaj zina maadili halafu Zigo ya AY haina maadili baasi unaacha tu iwe hivyo ,” aliongeza AY.
 
Pia AY alisema barua hiyo ilitoka kwa Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ikisema kwamba video hiyo inakiuka maadili.
Kwa mujibu wa Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungi, amethibitisha kuvitumia vituo vya luninga nchini taarifa ya namna ya kupembua kazi za wasanii zisizo na maadili.

Bilioni 4/-Zaokolewa kwa Kuzuia Safari za Ndani



OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeokoa Sh bilioni 4.38 ambazo zingetumika na watumishi wa Halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya safari za ndani.

Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene alibainisha hayo katika kipindi maalumu cha Siku 100 za Serikali ya Awamu ya Tano kinachorushwa na kituo cha televisheni cha TBC1 cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

“Katika kipindi cha siku 95, tumeweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo watumishi wa halmashauri wangezitumia katika safari za ndani zisizo na tija na hazijalenga kumkomboa mwananchi huyu ambaye hana dawa na hana barabara,” alisema Simbachawene.

Akizungumzia uwajibikaji wa watumishi katika halmashauri nchini, Simbachawene alisema ili kuhakikisha halmashauri hizo zinafanya kazi ipasavyo, wameunda kitengo cha ukaguzi ambacho kina kazi ya kudhibiti na kufuatilia utendaji wa kazi za halmashauri.

“Tamisemi tuna deni kubwa, kwani sisi ndio tunaotegemewa na wizara kutafsiri mipango yao ya elimu afya, miundombinu na sekta nyingine. Tamisemi ni wakala wa serikali kwa wananchi,” alisema na kuongeza kuwa watendaji wa halmashauri ambao hawataki kwenda na kasi ya Rais Magufuli, basi wataondolewa katika nafasi zao bila kuonewa haya.

“Tutahakikisha tunawachukulia hatua wezi wote, wabadhirifu na wasio waadilifu, huwezi utupishe. Tutawapima kwa jinsi wanavyoondoa kero kwa wananchi,” alisema na kukiri kuwa katika halmashauri kuna matatizo ya uadilifu jambo linalofanya miradi mingi kushindwa kukamilika na ikikamilika inakuwa chini ya kiwango.

Aidha, amewataka wakurugenzi kuhakikisha wanawafikia wananchi na kumaliza kero za wananchi kinyume chake kazi wataiona chungu.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato, Simbachawene alisema asilimia 95 ya halmashauri zote zimeanza kutumia mfumo wa elektroniki katika kukusanya mapato na kuwa zile chache ambazo hazijaanza zimetakiwa kufanya hivyo baada ya kuongezewa muda kidogo.

TBS Yawataka Wazalisha Nondo Kuanza Kuweka Lebo ( TBS steel bar ID & labelling )


Gavana Azindua Mwongozo Wa Kwanza Wa Kitaifa Wa Elimu Na Ulinzi Kwa Mtumiaji Wa Huduma Za Fedha (N-FEF).



Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kushirikiana na Mfuko wa Kuendeleza Huduma za Kifedha Tanzania (FSDT), imezindua Mwongozo wa taifa wenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu elimu ya mambo ya fedha kwa wananchi.

Uelimishwaji wa wananchi kuhusu mambo ya fedha utatekelezwa kupitia “Mwongozo wa kwanza wa kitaifa wa elimu na ulinzi kwa mtumiaji wa huduma za fedha” (N-FEF).

Gavana Prof. Beno Ndulu ameuzindua rasmi mwongozo huu ambao utajikita katika kutatua changamoto zilizobainishwa katika utafiti uliopima uelewa wa mambo ya fedha kwa watu wazima nchini Tanzania. Utafiti huu unaitwa “Uwezo wa Kifedha Tanzania” wa mwaka 2014.

Utafiti huo umebainisha kuwa watanzania wengi hawana elimu na ujuzi mahususi wa masuala ya mambo ya fedha kwa ujumla, hivyo kuwanyima fursa ya kutumia huduma za kifedha kwa faida yao.

Katika utafiti huo imeonyeshwa kuwa upatikanaji wa huduma za fedha umekuwa na changamoto katika maeneo mengi huku zile zitolewazo kwa njia ya mitandao bado hazikidhi matarajio ingawa zinawafikia wateja wengi kwa sasa.

Sambamba na hilo kumekuwa na uhaba wa nyenzo na miundombinu ya kuhifadhi na kufikisha taarifa za fedha kwa watumiaji wa huduma hizo kwa kuzingatia namna sahihi ya kutoa taarifa, kuwaelimisha na kuwalinda.

Kutokana na utafiti wa “Uwezo wa Kifedha Tanzania” wa mwaka 2014 wananchi kutoka makundi mbalimbali katika jamii hawana ujuzi wa hesabu za kawaida ambao ndiyo msingi mkuu katika nadharia ya masuala yahusuyo mambo ya fedha.

Elimu msingi katika masuala ya fedha umekuwa kikwazo kwa waliowengi hasa katika uandaaji wa bajeti, kutunza kumbukumbu ya matumizi, kupanga fedha kwa matumizi yasiyotegemewa ama ya ziada na muhimu zaidi kutunza kiasi kwa ajili ya matumizi ya uzeeni (baada ya kustaafu).

Inaonekana kuwa upatikanaji wa taarifa za masuala ya fedha hutegemea zaidi vyombo vya habari kama redio, televisheni na magazeti lakini vyombo hivi kwa sehemu kubwa, hufikisha zaidi taarifa za biashara na masoko kuliko ambavyo vinaelimisha jamii kuhusu matumizi na upangaji wa mapato yao.

“Haya ndiyo masuala mahususi ambayo mwongozo huu wa taifa kuhusu elimu ya huduma za fedha unalenga kushughulika nayo,” alisema Prof Ndulu.

Pamoja na kuwepo ongezeko la upatikanaji wa huduma za kifedha, mpaka asilimia 58 mwaka 2013 kutoka kiwango cha asilimia 17 mwaka 2009, miongoni mwa watu wazima nchini, bado mwongozo huu ni muhimu ili kuleta mfumo imara wa sekta ya fedha na Zaidi sana ili kuleta ustawi wa maisha ya watanzania kwa ujumla.

Prof. Ndulu anasema kutatua changamoto za kielimu kwa ujumla na hususan elimu ya huduma za fedha italiwezesha taifa kuwa katika mwelekeo mzuri wa kukabiliana na umasikini na kufikia malengo ya kukuza uchumi.

“Tunapaswa kujiuliza: ni kwa namna gani wananchi hasa wale masikini na wasiokuwa na elimu za kifedha za wanapambana kuendeleza biashara zao katika mazingira ya soko huria na lenye ushindani kila uchwao” alisisitiza Prof. Ndulu.

Hivyo, mwongozo huu utahakikisha watanzania wapata elimu sahihi na ya uhakika ya huduma za kifedha pamoja na njia anazoweza nazo kujilinda katika ushindani huu.

Vilevile mwongozo huu umeundwa ili kutatua changamoto za kifedha zinazohusiana na maamuzi miongoni mwa watumiaji wa huduma hizi na kuwa jumuishi na wenye tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Mwongozo wa taifa kuhusu elimu ya huduma za fedha umeandaliwa kwa kujumisha washikadau kutoka Tanzania bara na Zanzibar.

Unabainisha changamoto zinazohusuana na uwezo wa kifedha ambazo zinahitaji kutatuliwa kwa uwepo wa elimu ya fedha. Pia, unatoa taratibu wakufanikisha utekelezaji wa elimu ya fedha, na mwongozo wa kitaifa wa kuratibu elimu ya fedha nchini.

Lengo la mwongozo wa elimu ya huduma za fedha ni kuwa na wananchi na kaya zenye uwezo kifedha nchini.

Tuesday, February 23, 2016

Waziri Mkuu Majaliwa Awatembelea Waathirika Wa Mafuriko Iringa, Apokea Misaada Ya Maafa Ya Sh. Milioni 86/-


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea misaada mbalimbali yenye thamani ya sh. milioni 85.88/- kwa ajili ya wananchi walioathirika na mafuriko kwenye vijiji vya kata ya Mlenge, tarafa ya Pawaga,  wilaya ya Iringa vijijini mkoa wa Iringa. 
Misaada hiyo imetolewa na wadau mbalimbali kutokana na mafuriko ambayo yalibomoa nyumba 82 katika kitongoji cha Kilala, kijiji cha Kisanga na kuwaacha wananchi wake bila makazi. 
 
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kasanga ambako alikwenda kukagua athari za mafuriko  na kuwapa pole wananchi hao jana mchana (Jumatatu, Februari 22, 2016), Waziri Mkuu aliwashukuru wadau wote waliojitolea kuwachangia watu waliopata maafa kutokana na mafuriko hayo.
 
Wadau waliotoa misaada hiyo ni Benki ya NMB mabati 500, mifuko ya saruji 500, kilo 820 za maharage, kilo 750 za unga wa mahindi na lita 250 za mafuta ya kupikia vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 20/-. Wengine ni Mfuko wa Pensheni wa PPF uliotoa mabati 200 na mifuko ya saruji 200  vyenye thamani ya sh. milioni 6.6/-.
 
Wengine ni Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) waliotoa mabati 200 na mifuko ya saruji 160 vyenye thamani ya sh. milioni 4.5/-; Kiwanda cha kusindika nyanya cha RedGold kimetoa mifuko ya saruji 100 na mabati 50 vyenye thamani ya sh. Milioni 3/-; mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya CHADEMA, Bi. Susan Chogisasa na wenzake wametoa mabati 150, mifuko 23 ya saruji, kilo 100 za  maharage, kilo 50 za chumvi na nguo mbalimbali vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 1.3/-.

Madiwani wa Iringa Vijijini walitoa sh. 380,000/-, Wabunge wa Viti Maalum kupitia CCM walitoa vifaa vya sh. Milioni 1.7/-; ofisi ya CCM Mkoa wametoa vifaa vya sh. milioni 6.1/-, Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Iringa,  Bw. Salim Abri aliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Iringa sh. milioni 5/- ili wanunue vyakula vya waliopatwa na maafa.
 
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni mbunge wa Isimani, Bw. William Lukuvi alitoa fedha taslim sh. milioni  20/- kati ya hizo sh. milioni  15 zikiwa ni zake na milioni 5/- ni za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Bw. George Simbachawene.  Pia alikabidhi seti 251 za mashuka zenye thamani ya sh. milioni 4/- zikiwa ni mchango kutoka Benki ya CRDB.

Waziri Lukuvi ambaye alishatoa mabati 250, aliahidi kuongeza mabati mengine 250 (yote yana thamani ya sh. milioni 8), pia alikabidhi sh. milioni 1.5/- kwa diwani wa Mlenge ili ziwasaidie kukodi gari la kukarabati barabara yao ambayo imeharibika sana kutokana na mafuriko hayo. 
 
Mapema, akitoa taarifa ya maafa kwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bi. Amina Masenza alisema jumla ya kaya 82 zilikosa makazi kutokana na mvua zilizonyesha Februari 12 na kusababisha mafuriko. Kabla ya hapo, kaya nyingine 75 zenye wakazi 377ziliathirika kutokana na mvua zilizoanza Februari 3, mwaka huu. 
 
Alisema miundombinu ya barabara na ya maji safi iliharibiwa vibaya na kusababisha hasara ya zaidi ya sh, milioni 250/-. Pia wakazi hao walikumbwa na ugonjwa wa kipindupindu kutokana na mto Mapogoro kufurika na kusomba baadhi ya vyoo vya wakazi hao. 
 
“Tangu Februari mosi, wamekwishapokea wagonjwa wa kipindupinda 351 lakini walioko wodini hivi sasa ni wagonjwa 25 tu,“ alisema Mkuu huyo wa mkoa.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 22, 2016.
Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa akiwapa pole wanawake na watoto wakati alipotembelea makazi ya dharura  waliyojengewa na serikali katika kijiji cha Kasanga  wanapohifadhiwa waathirika wa mafuriko yaliyozikumba tarafa za Pawaga na Idodi , Iringa Februari 22, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akipokea taarifa ya msaada  kutoka kwa meneja uhusiano wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Lulu Mangele katika mkutano wa kuwapa pole wananchi wa tarafa za Pawaga na Idodi uliohutubiwa na Waziri Mkuu katika Kijiji cha Kasanga, Iringa Februari 22, 2016. Mfuko huo umetoa mabati 200 na saruji mifuko 200 vyote vikiwa na thamani ya sh. 6,600,000/=.
Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa akiwapa pole kinamama na watoto wakati alipotembelea makazi ya dharura  waliyojengewa na serikali katika kijiji cha Kasanga  wanapohifadhiwa waathirika wa mafuriko yaliyozikumba tarafa za Pawaga na Idodi , Iringa Februari 22, 2016.

Tuesday, February 23, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Jumanne Ya Februari 23



Tuesday, February 23, 2016

Serikali Yapanga Bei Elekezi Kwa Hospitali Binafsi Ili Kupunguza Mzigo wa Gharama



SERIKALI imesema itatoa bei elekezi katika sekta ya afya hivi karibuni baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kubariki bei hizo kuanza kutumika kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wa gharama wananchi.

Bei elekezi kwa vituo vya afya zimeshasainiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na baadhi ya vituo vya afya vimeshaanza kutumia bei hiyo.

Aidha, serikali imepanga kuweka utaratibu wa wagonjwa kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ikiwa ni hatua ya kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali hiyo.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk Hamis Kigwangalla wakati akizungumza na waaandishi wa habari baada ya kuzindua Matokeo ya Utafiti wa Kutathimini utoaji wa huduma za afya nchini kwa mwaka 2014/2015.

“Bei elekezi ziko mbioni kutoka na baadhi ya vituo wameshaanza kuzitumia kwa sababu zimeshasainiwa na Waziri, sasa hivi tunasubiri Baraka za Waziri Mkuu akiziridhia tutazitangaza rasmi,” alisema Dk Kigwangalla.


Tuesday, February 23, 2016

TRA Yatoa Tamko ya Kuhusu Matumizi ya EFD Kwenye vituo vya Mafuta.



TANGAZO KWA UMMA
MATUMIZI YA MASHINE ZA EFD KATIKA VITUO VYOTE VYA MAFUTA NCHINI:

Kufuatia Tangazo kwa Umma lilitolewa kwenye vyombo vya Habari na kuchapishwa kwenye Magazeti, Uongozi wa Chama cha Wamiliki na Waendeshaji wa Vituo vya Mafuta Nchini (TAPSOA) ulikutana na Kaimu Kamishna Mkuu na kufanya majadiliano ya msingi kuhusu matumizi ya EFD na kufunga Mashine za EFD Maalum katika vituo vya mafuta kwa ajili ya kutolea risiti za mauzo. Makubaliano ya pamoja kutokana na majadiliano ni kwamba, agizo la Kaimu Kamishna Mkuu liendelee kutekelezwa katika utaratibu ufuatao;
  1.  Wamiliki wote wenye vituo vya mafuta walio katika kundi la Makampuni makubwa wanaoagiza mafuta na kutumia Mawakala kusambaza/kuuza mafuta kwa wateja (CODO) wakamilishe kufunga Mashine za EFD katika vituo vyao vyote Nchini kama ilivyokubalika katika kikao hicho (yaani kufikia tarehe 15 Machi 2016).
  2.  Wamiliki wote wenye vituo vya mafuta walio katika kundi la Makampuni wanaoagiza mafuta na kusambaza/ kuuza mafuta kwa wateja wao wenyewe (COCO) walioanza na wanaofunga Mashine za EFD kwenye pampu za vituo vyao waendelee kufanya hivyo wakati Mamlaka ya Mapato kwa kushirikiana na Wasambazaji na Uongozi wa TAPSOA wakiendelea kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazojitokeza za kiufundi na gharama ya Mashine za EFD kwa ajili ya pampu husika.
  3. Wamiliki/Waendeshaji wote wenye vituo vya mafuta walio katika kundi la Makampuni ya watu binafsi wanaonunua mafuta kutoka kwa Makampuni mama na kusambaza/kuuza kwa wateja moja kwa moja (DODO) ambao hawajafunga Mashine za EFD kwenye pampu waendelee kutumia Mashine za EFD za kawaida (ETR) wakati changamoto za kiufundi, mtandao na bei za Mashine za EFD zikishughulikiwa.
Mamlaka ya Mapato kwa kushirikiana na uongozi wa TAPSOA kwa pamoja tutaendelea kuhimiza Matumizi ya Mashine za EFD katika vituo vya mafuta vyote Nchini.

Ni vyema kila Mfanyabiashara akatambua wajibu wake na kujenga utamaduni wa kutekeleza matakwa ya sheria kwa hiari bila kushurutishwa.

Pamoja Tunajenga Taifa Letu
KAIMU KAMISHNA MKUU

Meneja wa Shirika la Posta Tanzania Afikishwa Mahakamani Kwa Matumizi Mabaya Ya Ofisi



Meneja wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Mkoa wa Dar es Salaam, Lawrence Mwalumwelo na wenzake wawili wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Sophia Nyanda akishirikiana na Veronica Chimwanda mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni Ofisa Tawala, Modester Fumbuka na Ofisa Manunuzi, Radecunda Massawe, wafanyakazi wa TPC.

Chimwanda alidai kuwa kati ya Agosti Mosi na Oktoba 31, 2010 washtakiwa hao walitumia vibaya madaraka yao kwa kuipa mkataba wa kutafuta vibarua kampuni ya Technical Merchantile Service bila kupata kibali kutoka bodi ya zabuni.

Vilevile ilidaiwa kuwa Septemba 26 ,2011 washtakiwa hao walitumia vibaya madaraka yao kwa kuiongezea kampuni hiyo mkataba wa kutafuta vibarua kutoka Septemba 30 hadi Desemba 31, 2011 bila ya kuishirikisha bodi hiyo.

Ilidaiwa kuwa Januari Mosi, 2012 washtakiwa hao waliiongezea tena kampuni hiyo mkataba wa kutafuta vibarua kutoka Januari Mosi, 2012 hadi Machi 30, 2014 bila ya kuishirikisha bodi hiyo. Washtakiwa hao walikana mashtaka.

Washtakiwa hao waliachiwa baada ya kutumiza masharti ya dhamana na kesi hiyo kuahirishwa hadi Machi 17.

CCM Watuma Salamu za Pongezi Kwa Yoweri Museveni Kwa Ushindi wa Kiti cha Urais Uganda


Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepongeza Chama cha National Resistance Movement (NRM) cha nchini Uganda kwa ushindi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Februari 18.

Kutokana na ushindi huo  CCM inampongeza Rais mteule, Yoweri Museveni ambaye ndiye mwenyekiti wa NRM.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma wa CCM, Daniel Chongolo imeeleza kuwa wamefuatilia kwa ukaribu mchakato wa uchaguzi huo na walikuwa na imani kwamba NRM itaibuka mshindi dhidi ya waliokuwa wagombea wengine saba wa urais. 
===== 

Mwanamkakati wa Maalim Seif Aswekwa Ndani Na Jeshi La Polisi Zanzibar


Mwanamkakati  wa aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, Mohamed Sultan Mugheiry, maarufu kwa jina la Eddy Riyami, amewekwa ndani na Jeshi la Polisi mjini Unguja kwa tuhuma za kumtukana Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Eddy Riyami ambaye ni mmoja wa wana mkakati wa timu ya ushindi wa aliyekuwa mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alikutwa na mkasa huo jana baada ya kuitwa polisi kutoa maelezo kutokana na tuhuma zinazomkabili.

Riyami ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, alikwenda Polisi Makao Makuu kuitikia wito wa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, SSP Simon Pasua, huku akiandamana na Mwanasheria wa CUF, Masoud Faki Masoud.

Mwanasheria huyo jana alisema Riyami anatuhumiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya kimtandao.

Alisema licha ya kuzikana tuhuma hizo, lakini Jeshi la Polisi bado lilimshikilia kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

“Ni kweli ameshikiliwa na polisi kwa ajili ya kupitisha uchunguzi na yupo Polisi Madema, eti Eddy kaambiwa kamtukana Dr. Shein kwenye ‘audio’ ambayo hata si sauti yake, lakini dhamana ipo wazi na tutamchukulia dhamana,” alisema Masoud.

Akizungumzia kukamatwa kwa Riyami, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Salum Msangi, alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

“Kitu ninachoweza kuthibitisha ni kuwa tunamshikilia Riyami kwa ajili ya kupitisha uchunguzi,” alisema Naibu Kamishna Msangi.
 
Februari 15, mwaka huu Ofisi ya Mkurunzi na Makosa ya Jinai, ilimwandikia Riyami barua ya wito na kumtaka kufika ofisi ya upelelezi iliyopo Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.

Riyami alitii wito huo ambapo wiki iliyopita alikwenda lakini mmoja wa maofisa wa Jeshi la Polisi aliyemwandikia barua alikuwa nje ya Zanzibar kwa shughuli za kikazi na kumtaka kwenda jana jumatatu

Riyami si mwanachama wa CUF, lakini mara kadhaa amekuwa akitumiwa na chama hicho kwa ajili ya mikakati mbalimbali pamoja na ushauri.