Friday, March 18, 2016


Friday, March 18, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Ijumaa ya March 18


Thursday, March 17, 2016

Wednesday, March 16, 2016

Mkuu Mpya Wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali mstaafu Salum Mustafa Kijuu Atoa Onyo Kali Kwa Majambazi na Wahalifu.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali mstaafu Salum Mustafa Kijuu amewataka watu wote wanaopindisha sheria, majambazi na wahalifu wote kutafuta kazi nyingine halali za kufanya.

Meja Kijuu aliyasema hayo baada ya kula kiapo cha utiifu na uadilifu kuwatumikia wananchi wa mkoa wa Kagera mkoa ambao upo pembezoni mwa nchi unaokabiliwa na matukio ya mara kwa mara ya uhalifu.

''Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyonayo kwangu na nitafanya kazi kwa kuzingatia yale ambayo ameyasema na kuhakikisha maendeleo yanapatikana''-Amesema Meja Kijuu

''Sitakubali watu wazurure hovyo na kuacha kufanya kazi za uzalishaji na nitahakikisha napambana na wahalifu wote kwa uwezo wote nilionao"-Amesisitiza Meja Kijuu.

Aidha Rais Magufuli aliwaapisha wanajeshi wastaafu Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Elias Kyunga, aliyekuwa Chuo cha Kamanda na Unadhimu (JWTZ) ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu, aliyekuwa Mkuu wa Kamandi ya Nchi Kavu ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Wengine ni Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi na Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga, aliyekuwa Makao Makuu ya Jeshi sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma 

Lengo la Rais kuweka wanajeshi katika mikoa ya pembezoni ni kuleta usalama na kuimarisha amani katika mikoa hiyo.

Wednesday, March 16, 2016

Rais Magufuli Akagua Na Kuweka Jiwe La Msingi Katika Ujenzi Wa Kituo Cha Kufua Umeme wa Megawat 240 Cha Kinyerezi II Jijini Dar Es Salaam Marchi 16,2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Balozi wa Japan nchini Masaharu Yoshida, Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam CCM, Ramadhan Madabida, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Juliana Palangyo wakikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Ujenzi wa Kituo cha Kufua umeme cha Kinyerezi II nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Balozi wa Japan nchini Masaharu Yoshida , Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, Mkurugenzi mkuu wa Tanesco Felchesmi Mramba wakivuta utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Ujenzi wa Kituo cha Kufua umeme cha Kinyerezi II nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisikiliza maelezo kutoka Meneja wa Kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi I Mhandisi John Mageni kuhusu utendaji kazi wa kituo hicho.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akitoa maelekezo kwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kuhusu ujenzi wa Kituo cha Kufua umeme cha Kinyerezi I nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
 Meneja wa Kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi I Mhandisi John Mageni akitoa maelekezo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu mitambo ya kufua umeme kwa kinyerezi I nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa kinyerezi hawapo pichani kabla ya kuzindua rasmi Ujenzi wa Kituo cha Kufua umeme cha Kinyerezi II nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Mkurugenzi mkuu wa Tanesco Felchesmi Mramba akifafanua jinsi ujenzi wa Kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi II kitakavyokuwa mara baada ya kukamilika mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam CCM Ramadhani Madabida kabla ya uzinduzi wa uzinduzi rasmi wa Ujenzi wa Kituo cha Kufua umeme cha Kinyerezi II nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, Balozi wa Japan Nchini Masaharu Yoshida, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ,Mama Janeth Magufuli wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa TANESCO mara baada ya kuzindua rasmi ujenzi wa Kituo cha Kufua umeme cha Kinyerezi II nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza kwa makini mama mmoja alijitokeza kumpongeza kutokana na utendaji kazi mzuri wa Serikali yake ya awamu ya tano mara baada ya uzinduzi rasmi ujenzi wa wa Kituo cha Kufua umeme cha Kinyerezi II nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati alipowasili kwenye ofisi za kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi I nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Wananchi wakishangilia wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa akiwahutubia huko Kinyerezi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam


Thursday, March 17, 2016

Rais Magufuli Apiga MARUFUKU Kukodi Mitambo ya Kuzalisha Umeme


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 16 Machi, 2016 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi namba mbili, uliopo katika wilaya ya Ilala Mkoani Dar es salaam, ambao utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawatts 240 za umeme.
 
Mradi huo ambao utazalisha umeme kwa kutumia gesi asilia inayosafirishwa kwa bomba kutoka Mtwara, unatarajiwa kuanza kuzalisha umeme katika kipindi cha kuanzia miezi 21 hadi 28 utakapokamilika kabisa.
 
Kuanza kwa ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme huo, kunafuatia juhudi zilizofanywa na serikali ya awamu ya tano ya kufanikisha upatikanaji wa shilingi bilioni 120, ikiwa ni asilimia 15 ya fedha zilizopaswa kutolewa na Tanzania na fedha nyingine shilingi Bilioni 292 zimetolewa na Japan.
 
Mradi huu umetanguliwa na mradi wa Kinyerezi namba moja ambao una uwezo wa kuzalisha megawatts 150 za umeme, na mitambo yake tayari imeanza uzalishaji wa megawatts 105 zilizoingizwa katika gridi ya Taifa.
 
Pamoja na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa Kinyerezi namba mbili, Rais Magufuli amekagua mitambo ya kuzalisha umeme ya mradi wa Kinyerezi namba moja, ambapo Mkuu wa Kituo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) cha Kinyerezi Mhandisi John Mageni, ametoa maelezo kuwa shirika hilo lina mpango wa kupanua uzalishaji wa umeme katika mradi huo kutoka megawatts 150 hadi kufikia megawatta 335, kwa kuongeza mitambo ya kufua umeme kwa teknolojia inayojumuisha matumizi ya gesi asilia na mvuke uzalishwao na mitambo hiyo.
 
Baadaya ya kupokea maelezo hayo, Rais Magufuli ameridhia kuwa serikali yake itatoa Dola za kimarekani milioni 20, kwa ajili ya kufanikisha upanuzi wa mradi huo na ameagiza kuwa wataalamu wa TANESCO washirikiane na Mkandalasi kuhakikisha upanuzi huo unafanyika haraka iwezekanavyo, badala ya muda wa miezi 12 uliopangwa.
 
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika sherehe za uzinduzi wa mradi huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO, kuanza kuachana na mitambo ya kukodi kwa ajili ya kuzalisha umeme, na badala yake nchi ijenge mitambo yake yenyewe ili kuondokana na gharama kubwa za nishati hiyo muhimu.
 
“Waziri, ukiona mtaalamu anakuletea mapendekezo ya kutaka kukodi mitambo ya kuzalisha umeme, badala ya kuleta mapendekezo ya kununua mitambo yetu wenyewe ujue mtaalamu huyo hafai, mtoe” Amesisitiza Rais Magufuli
 
Ameongeza kuwa tafiti zimethibitisha kuwa hadi sasa Tanzania ina zaidi ya futi za ujazo Trilioni 57 za gesi asilia, ambayo itazalisha umeme wa kutosheleza mahitaji ya ndani, na umeme mwingine kuuzwa nje ya nchi ikiwemo Kenya ambayo tayari imeomba kuuziwa umeme kutoka Tanzania.
 
Aidha, Rais Magufuli ametoa onyo kwa TANESCO kuwa hatarajii kusikia bwawa la maji la Mtera limeishiwa maji, kwa kuwa katika msimu huu wa mvua maeneo ya Iringa yalikuwa na mvua nyingi ambazo zimesababisha hadi mafuriko mafurukio.
 
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo amesema tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, juhudi zilizofanyika zimefanikisha kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawatts 800 hadi kufikia megawatts 1,000 kiasi ambacho ni pungufu kwa megawatts 20 tu, ikilinganishwa na mahitaji ya megawatts 1020 za sasa.
 
Ameongeza kuwa pamoja na kuweka jiwe la msingi la mradi wa Kinyerezi namba mbili, hivi karibuni serikali inatarajia kujenga miradi mingine ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia, ikiwemo Kinyerezi namba tatu utakaozalisha megawatts 600, Kinyerezi namba nne utakaozalisha megawatts 300, na mingine itakayojengwa Lindi na Mtwara.
 
Prof. Muhongo amebainisha kuwa mpaka sasa gesi asilia inazalisha kati ya asilimia 50 na 60 ya umeme wote hapa nchini, Maji yanazalisha asilimia 30 hadi 40, na umeme unaozalishwa kwa mafuta hauvuki asilimia 10.
 
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Balozi wa Japani hapa nchini Mheshimiwa Masaharu Yoshida, Wabunge wa kamati ya Nishati na Madini, wafadhili wakiwemo Benki ya Dunia, Benki ya Afrika na Shirika misaada la Japan (JICA.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
16 Machi, 2016
Thursday, March 17, 2016

Rais Magufuli Akerwa Na Mikataba Mibovu Ya Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL....Aeleza Kilichomfanya Amrudishe Profesa Muhongo Wizara ya Nishati


Rais John Magufuli jana aliitaja kampuni ya kuzalisha umeme ya IPTL wakati akizungumzia matatizo yanayosababishwa na kununua umeme unaozalishwa na mitambo ya kukodi na kupiga marufuku mikataba hiyo. 
Rais pia alipuuzia shutuma zinazorushwa dhidi ya Profesa Sospeter Muhongo, ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri wa Nishati na Madini kutokana na sakata la IPTL, akisema “wakati mwingine vitu vizuri hupigwa vita” na hivyo amemrejesha mbunge huyo wa Musoma Vijijini kwenye wizara hiyo kwa sababu ya uchapakazi na si siasa.
 Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amekuwa akifichua kashfa za ufisadi ambazo hazikuwahi kujadiliwa vikali katika utawala uliopita, lakini jana alitoa mfano wa IPTL kama moja ya mikataba iliyoisababishia Serikali matatizo. 
Kashfa zilizoikumba sekta hiyo ni pamoja na mkataba wa uzalishaji umeme na kampuni ya Richmond Development iliyodhihirika baadaye kuwa haikuwa na uwezo, uchotwaji wa zaidi ya Sh300 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyohusisha IPTL, mikataba ya ununuzi umeme kwa bei kubwa kutoka kampuni binafsi na ununuzi wa umeme kutoka mitambo ya kukodi.

“Ni matumani yangu kuwa sitasikia tena mnaleta mapendekezo kwamba tunataka kuongeza mkataba huu au tunataka kukodi mtambo huu.Suala la kukodi likalegee, lizimie na life kabisa huko,” alisema Rais Magufuli wakati akizindua ujenzi wa kituo cha umeme cha mradi wa Kinyerezi ll utakaokuwa ukizalisha megawati 280 kwa mwaka jijini Dar es Salaam jana.
“Hayo mawazo yafe, sasa tuwe na mawazo ya kujenga mitambo yetu. Cha kuazima ni kibaya. Hivi sasa vya kukodi na vya kuazima achaneni navyo. Nendeni na mawazo ya kujenga mitambo yetu.

“Tumechoka kuchezewa. Kuna miradi hapa ya hovyo kweli. Kila siku inazaa matatizo. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri (Muhongo) lisimamie hilo. " Alisema Rais Magufuli

Alisema Profesa Muhongo akipata ushauri kutoka kwa wataalamu wake kuhusu miradi ya kukodi mitambo, atambue kuwa hawafai. “Ujue huyo si mtaalamu mzuri, ikiwezekana mtoe. Wataalamu wako wakuletee mawazo ya kujenga mitambo yetu,” alisema. 
Rais Magufuli alisema ni lazima ufike wakati Tanzania iwe na umeme wa uhakika tena wa kujitegemea.

 “Si umeme kwa kukodisha- kodisha. Umeme ni wa kutumia watu. Na ndiyo maana kumekuwa na matatizo mengi. Mara IPTL mara nini. Ni kwa sababu tulizoea umeme wa kukodisha kwa wafanyabiashara,” alisema. 
Kampuni ya IPTL iliingia kwenye mgogoro na Serikali baada ya kudaiwa kuwa inaitoza Tanesco tozo kubwa gharama za uwekezaji kuliko makubaliano ya mkataba. 
Wakati wa kashfa ya escrow, zaidi ya Sh300 bilioni zilizokuwa zimewekwa kwenye akaunti hiyo kusubiri kumalizika kwa mgogoro wa kimkataba baina ya IPTL na Tanesco zilichotwa na kuonekana zikiingia kwenye akaunti za mawaziri, majaji, wabunge na watumishi waandamizi wa Serikali, jambo lililolifanya Bunge limlazimishe Profesa Muhongo awajibike kwa kushindwa kusimamia fedha za Serikali. 
 Profesa Muhongo alijiuzulu, lakini akateuliwa na Rais Magufuli kurudi kwenye nafasi hiyo na jana mkuu huyo wa nchi hakusita kummwagia sifa. 

 “Wizara ya Nishati mmenifurahisha sana. Tuachane na mitambo ya kukodi. Tumechoka kufanya biashara na wawekezaji wa ajabu ajabu. Halafu tunalipia capacity charges za ajabu na umeme unakuwa juu. Tunawapa shida Watanzania wa maisha ya chini,” alisema Magufuli. 
“Nendeni kwa kasi ya hapa kazi tu. Na ndiyo maana niliamua kumrudisha Profesa Muhongo hapo. Wakati mwingine vitu vizuri vinapigwa vita. Sichagui mwanasiasa. Mimi nataka mtu mchapa kazi. Maendeleo hayana chama.”
Akizungumzia ujenzi wa kituo cha Kinyerezi ll utakaogharimu dola 344 za Marekani (sawa na Sh688 bilioni), Rais alisema amefarijika kuona ndani ya muda wake mfupi akiwa madarakani amealikwa kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo.
 Alisema Serikali ya Japan ilitoa dola 292 milioni za Marekani na Tanzania ilitakiwa kutoa dola 52 milioni za Marekani sawa na asilimia 15, lakini ikashindikana na kutakiwa wasubiri. 
“Baada ya makusanyo kuimarika tulipoingia madarakani mwezi Novemba na Desemba mwaka jana, tulitoa maelekezo na hizo dola 52 milioni sawa Sh110 bilioni za Tanzania na zikapatikana ndiyo maana leo tupo hapa kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya mradi huu kuanza,” alisema.
 “Hivi sasa tuna uwezo wa kuzalisha megawati 1,200 hadi 1,500 za umeme kwa mwaka. Sasa tumefikia 1026. Hiyo ina maana kuwa kila Mtanzania kwa sasa anatumia wastani wa wati 30 kwa mwaka,” alisema. 
Pia alisema amefurahi kupata taarifa kuwa mradi ya Kinyerezi l utaongezewa uwezo wa uzalishaji kutoka megawati 150 hadi 335. 
“Nimeambiwa mkandarasi anataka dola 20 milioni za Marekani (sawa na Sh 40 bilioni). Sasa kama tuliweza kutoa hela kwa ajili ya Kinyerezi II, hatuwezi kushindwa kuongeza kwa ajili ya Kinyerezi l. Hiyo hela tutatafuta hata mwezi huu tutampa,” alisema.
Thursday, March 17, 2016

Kiongozi wa CUF Aliyetangaza Kuwa Wafuasi wa Chama Hicho Wamekimbilia Porini Akamatwa na Polisi


Ikiwa ni siku tatu tangu Mkurugenzi wa Habari Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Masoud Hamad, atangaze kuwa baadhi ya wananchi wa Zanzibar wanakimbilia porini kuhofia usalama wao, ametiwa mbaroni.

Kukamatwa kwa Masoud sasa kunafanya idadi ya viongozi wa chama hicho waliotiwa mbaroni na kuhojiwa polisi kufikia wanne tangu kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka jana.

Viongozi wengine waliohojiwa na Polisi na kuachiwa kwa dhamana ni Naibu Katibu Mkuu, Nassor Ahmed Mazrui, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Omar Alin Shehe na mshauri wa mikakati wa chama hicho, Eddy Riyami.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis Mkadam, jana alithibitisha kukamatwa kwa Masoud, ambaye ni Waziri wa zamani wa Miundombinu na Mawasiliano katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Alisema kiongozi huyo alikamatwa na kitengo cha upelelezi nyumbani kwake mtaa wa Mbweni mjini Zanzibar jana.

Alisema kwa sasa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Mwembe Madema ili kusadia uchunguzi juu ya taarifa alizotoa katika mkutano wake na waandishi wa habari na kuzungumzia hali ya amani ya Zanzibar na wananchi wake.

“Tunamshikilia kwa uchunguzi, kuna mambo ya msingi tunaona yanahitaji kufanyiwa uchunguzi na yeye kusadia polisi uchunguzi wake,” alisema Mkadam.

Kufuatia kukamatwa huko kwa Masoud, CUF imelaani kitendo hicho na kusema kuwa kamata kamata hiyo inawalenga viongozi wa chama hicho na wanachama wake pekee.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Mazrui alisema matukio yote ya uvunjifu wa amani yaliyotokea visiwani hapa, yamekuwa yakihusishwa  na CUF na Jeshi la Polisi huwakamata viongozi wa chama hicho pekee.

“Tunasema huu ni uonevu wa hali ya juu, maana viongozi na wafuasi wa CUF pekee ndio wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi, hii yote inatokana na uchaguzi wa marudio, hivyo  kutoshiriki kwetu kwa uchaguzi isiwe sababu ya kuadhibiwa,” alisema.

Aidha, alisema suala la kushiriki au kutoshiriki katika uchaguzi ni hiari ya mtu, hivyo kwa wale ambao hawatashiriki uchaguzi huo, wasiadhibiwe wala wasidhalilishwe na wale ambao wametangaza kushiriki waende wakapige kura.

Kwa upande wa mke wa Masoud, Rahma Issa, alisema askari kazu wasiopungua sita wakiwa na silaha za moto mbili walifika nyumbani jana saa moja asubuhi na kudai wanamhitaji mumewe.

Alisema baada ya kubisha hodi, kijana wake mmoja alifungua mlango na kisha askari watatu waliingia ndani mmoja akiwa na silaha ya moto kifuani.

“Baada ya kuamshwa na kutoka chumbani walimwambia yupo chini ya ulinzi anahitajika kituo cha polisi,” alisema Rahma.

Hata hivyo, alisema baada ya kumkamata, hawakumwambia sababu ya kukamatwa kwake, lakini baada ya kuwauliza wanampekeka kituo gani walimwabia Kituo cha Polisi Mwembe Madema, Zanzibar.

Naye Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alisema vitendo vya kukamatwa viongozi wa CUF ni mwendeleo wa Serikali ya CCM kuwanyanyasa viongozi na wanachama wake chama hivyo visiwani hapa.

Alisema vitendo vnavyoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi vinakwenda kinyume cha misingi ya demokrasia na haki za binadamu.

Shehe alisema matunda ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya kujenga amani na umoja wa kitaifa yameanza kuvurugwa tangu kuingia mgogoro wa uchaguzi mkuu.

Thursday, March 17, 2016

Habari Zilizopo Katika Magazeti Ya Leo Alhamisi Ya March 17