Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Akabidhiwa zana ya ‘Kisukuma’ Kukabili MAJIPU......Pia Kapewa Jina Jipya ambalo ni Masanja Mkusanyaji
WAZIRI
Mkuu Kassim Majaliwa amepewa jina jipya la Kisukuma na kukabidhiwa zana
nyingine muhimu katika vita ya kupambana na ufisadi nchini maarufu kwa
jina la kutumbua majipu.
Kuanzia juzi, Waziri Mkuu Majaliwa atakuwa akifahamika kwa jina lingine la Masanja, alilopewa na Wazee wa Kisukuma wa Lamadi wilayani Busega katika mkoa wa Simiyu.
Kabla
ya kuwahutubia maelfu ya wakazi wa Lamadi juzi jioni, wazee hao
walimvisha Waziri Mkuu vazi la kijadi la Kisukuma akiwa katika kigoda,
wakamkabidhi usinga, ng’ombe wawili na mkuki ambao walimueleza kuwa kazi
yake ni kuendeleza vita ya ufisadi kwa kuutumia kutumbua majipu.
“Tunakukabidhi
usinga na huu mkuki utumike kutumbua majipu kwa sababu kazi hii
unaifanya vizuri hadi sasa, kwa hiyo uendelee kutumbua majipu. Na kwa
kuanzia sasa, tunakupa jina la kwetu, kwa sababu wewe ni kijana wetu,
utaitwa Masanja,” alisema Mchele Malale kwa niaba ya wazee wenzake.
Kwa
mujibu wa wenyeji, jina la Masanja lina maana ya kuingia kokote, hali
inayomaanisha kuwa Waziri Mkuu Majaliwa aendelee kutumbua majipu kila
mahali.
Alipoanza
kuhutubia, Waziri Mkuu alikiri kuwa amepata mapokezi makubwa kwa
wananchi wa Lamadi, na zaidi, makubwa kuliko sehemu nyingi alizokwenda
tangu ashike wadhifa wake huo.
“Kwa
kweli nimefurahishwa na mapokezi yenu hapa…tangu nilipotoka Mwanza hadi
kufika kwenu (Busega) mapokezi yamekuwa mazuri, na hapa Lamadi
mmetisha. Mmenitia faraja sana,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza:
“Lakini
nimefurahi kwa zawadi mlizonipa na pia jina jipya la Masanja.Nimeandika
pale kwenye diary (shajala) yangu. Mmenipa pia mkuki, mmesema nitumie
kama sindano kuendeleza ile kazi,” alisema Waziri Mkuu na kushangiliwa na maelfu ya wakazi wa Lamadi.
Akiwa
Bariadi jana, Waziri Mkuu alisema jina lake sasa ni Masanja Mkusanyaji,
na kwamba ataendelea kukabiliana na wakwepa kodi na mafisadi ili
Watanzania wapate huduma stahiki.
No comments:
Post a Comment