Wednesday, March 9, 2016
Kubenea Akana Kumtukana Paul Makonda....Kesi Yaahirishwa Hadi March 10
Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea ameiambia Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu hakutoa lugha chafu dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,
Paul Makonda kama inavyodaiwa.
Kubenea alitoa kauli hiyo jana
wakati akitoa utetezi huku akiongozwa na wakili wake, Peter Kibatala
mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
“Mimi sijasema hayo
maneno kuwa Makonda ni mjinga, mpumbavu, kibaka na cheo chenyewe cha
kupewa, bali nilimwambia wewe umeteuliwa na Rais na mimi nimechaguliwa
na wananchi,” alidai.
Kubenea aliendelea kudai kuwa Desemba 14,
2015, katika kiwanda cha Tooku Garments Co. Ltd kilichopo Mabibo
External kwenye mgomo wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, alimwambia
Makonda hawezi kufunga mkutano bila ya yeye kuzungumza kwa sababu ni
mwakilishi wa wananchi.
Alidai kuwa Makonda alimjibu kila
alipokuwa akizungumza kuwa yeye ndiye mtu wa mwisho kwa kuwa ni rais wa
Kinondoni.
“Nilimjibu na mimi ni mbunge, nimeteuliwa na wananchi, lazima
aheshimu uwapo wangu pale,” alidai.
Kubenea alidai kutokana na
msimamo wa Makonda wa kutotaka kumpa nafasi ya kuzungumza na
wafanyakazi, alimwambia hajavamia mkutano huo bali aliitwa.
“Nikamwambia
mimi siyo kibaka bali nimechaguliwa na watu, baada ya kauli hiyo,
alimuamuru Mkuu wa Upelelezi wa Kituo cha Polisi Magomeni, Denis
anikamate nikapumzishwe mahabusu,” alidai.
Alidai kuwa mkuu huyo
wa wilaya, aliamuru pia kukamatwa kwa raia mmoja wa China anayedaiwa
kuwanyanyasa wafanyakazi hao ili achunguzwe.
Kesi hiyo itaendelea Machi 10, mwaka huu. Kubenea anadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 14, 2015 katika Kiwanda hicho.
No comments:
Post a Comment