Friday, March 4, 2016
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Nassor Ahmed Mazrui Ahojiwa na Jeshi la Polisi Zanzibar Na Kuachiwa Kwa Dhamana
Wakati
polisi visiwani Zanzibar wakimhoji Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor
Ahmed Mazrui jana, ulinzi uliimarishwa mjini Unguja huku askari wenye
silaha na magari ya deraya wakifanya doria mitaani.
Mazrui,
ambaye alifika makao makuu ya jeshi hilo saa 2:00 asubuhi akiambatana
na wakili wake, ndiye aliyekuwa mkuu wa timu ya kampeni ya mgombea urais
wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, katika uchaguzi uliofanyika tarehe 25
Oktoba 2015, ambao chama chake kinaamini kuwa kilishinda.
Barabara
zinazoelekea makao makuu ya polisi kutokea Jang’ombe, Kilimani na
Bomani zilifungwa huku vikosi vya ulinzi na usalama vikiwa vimetapakaa
maeneo hayo na mitaa mbalimbali mjini Unguja.
Wakazi
wa Zanzibar wanaojiandaa kwa uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika
Machi 20, kuanzia Jumatano mchana walishuhudia askari wenye sare wakiwa
katika magari maalumu ya kijeshi wakirandaranda kwenye barabara za
Unguja, hususan mitaa ya Ng’ambo kupitia Mnazi Mmoja, Darajani, Amani,
Chumbuni na Mtoni kuelekea Bububu.
Wakati
hali ikionekana hivyo mitaani, Mazrui alikuwa ndani ya Ofisi ya
Upelelezi ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Ziwani mjini Unguja ambamo
alihojiwa kwa saa tatu na nusu.
Alianza
kuhojiwa tangu saa 2.00 asubuhi kama alivyotakiwa na jeshi hilo
kuripoti kupitia barua ya wito aliyotumiwa hivi karibuni, hadi saa 5.30
Hata
baada ya kumaliza kuhojiwa, Mazrui aliyekuwa waziri wa biashara,
alilazimika kubaki kituoni hapo akisubiri kukamilika kwa taratibu za
dhamana. Aliruhusiwa kuondoka saa 6.40 mchana.
Pamoja
na ulinzi kuimarishwa, mamia ya wananchi, hasa wapenzi, wanachama na
wafuasi wa CUF, walifika makao makuu ya chama hicho yaliyoko Mtendeni
ili kumpokea Mazrui akitokea polisi.
Baada
ya kuachiwa kwa dhamana, Mazrui alisema alihojiwa na polisi kuhusu
kauli aliyoitoa hivi karibuni alipokuwa Dunga Kiembeni, Wilaya ya Kati
mkoani Kusini Unguja kwamba chama chake cha CUF kimechoshwa na vitendo
vya hujuma na vya kihuni dhidi ya mali na ofisi zao.
“Naam, nimewaambia kwamba hiyo ni kauli yangu na niliyesema hayo ni mimi kuwa CUF tumechoshwa na uhuni huo,” alisisitiza
Mazrui mara baada ya kuachiwa kwa dhamana ya masharti ya kuwa na
wadhamini wawili na kila mmoja wao kutakiwa kuweka hapo Sh500,000.
“Wamesema nimetoa kauli za uchochezi hivyo watanishtaki mahakamani na wamenitaka niripoti polisi Jumanne na Alhamisi.” Alisema
No comments:
Post a Comment