Friday, February 5, 2016
Serikali Yalaani Kitendo Cha Kudhalilishwa Kwa Mtanzania Nchini India
Serikali
ya Tanzania imesikitishwa na inalaani vikali kitendo cha udhalilishwaji
alichofanyiwa mwanafunzi wa kike wa Kitanzania na Kundi la watu katika
jimbo la Bangalore nchini India.
Kauli
hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje,
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Ramadhani
Muombwa Mwinyi alipokutana na Wandishi wa Habari kwa ajili ya kuwaeleza
hatua zilizochukuliwa na Serikali kufuatia kitendo hicho cha
kudhalilishwa kwa mwanafunzi wa Kitanzania nchini India.
Balozi
Mwinyi alisema kuwa, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na Ubalozi wa
Tanzania nchini India kuiandikia Serikali ya nchi hiyo kuomba maelezo
kamili kuhusu tukio hilo pamoja na kuitaka Serikali ya India
kuwachukulia hatua za kisheria watu wote waliohusika pamoja na
kuimarisha usalama katika maeneo wanayoishi wanafunzi wa Kitanzania.
Aidha,
Balozi Mwinyi alieleza kuwa amemwita Balozi wa India hapa nchini, Mhe.
Sandeep Arya na kumweleza masikitiko ya Serikali ya Tanzania kufuatia
kitendo hicho cha kushambuliwa na kudhalilishwa kwa mwanafunzi wa kike
kutoka Tanzania.
Katika
mazungumzo yao, Balozi Arya alieleza bayana kuwa Serikali ya India
imesikitishwa na tukio hilo la udhalilishaji na kwamba Serikali imeahidi
kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kutekeleza uovu
huo.
Alisema
kuwa Waziri Mkuu wa Jimbo la Bangalore aliongea na umma kuelezea
masikitiko yake kuhusu uovu huo na kuahidi kuwa mamlaka za jimbo hilo
zitaimarisha usalama katika maeneo yote wanayoishi wanafunzi wa Tanzania
na raia wengine kutoka nje.
Balozi
Arya aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa India inaheshimu
ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na nchi yake, hivyo itashughulikia
suala hilo kwa ukamilifu na hadi wakati huu tayari watu watano
wanashikiliwa na vyombo vya usalama wakituhumiwa kuhusika na tukio hilo.
Sanjari
na taarifa hiyo, Balozi Mwinyi aliwaomba Watanzania kutohusisha tukio
hili la uhalifu na ajali ya Mtanzania, Bw. Christian Benjamin Mlyansi
iliyotokea nchini India jana usiku na kusababisha kifo chake.
Alisema
kuwa Bw. Mlyansi alipata ajali ya kawaida alipokuwa anaendesha pikipiki
ambapo ilipoteza mwelekeo na kugonga ukingo wa kati wa barabara.
Thursday, February 4, 2016
Mke wa Kafulila atimuliwa nje ya ukumbi wa bunge
Mbunge
wa Viti maalum Chadema Jesca Kishoa ametolewa nje ya ukumbi wa bunge na
kutakiwa kutohudhuria vikao viwili vya bunge linaloendelea mjini
Dodoma.
Hayo
yamejiri katika mkutano wa 7 wa bunge la 11 linaloendelea na vikao
vyake mjini Dodoma ambapo Mwenyekiti wa kikao cha leo Andrew Chenge
amelikumbusha bunge kuhusiana na kauli aliyoitoa mbunge huyo tarehe
01/02/2016.
Mbunge
huyo alisema kwamba Waziri Harrison Mwakyembe alihusika kununua
mabehewa feki 274 jambo ambalo lilizua mjadala mkali na bunge kumtaka
mbunge huyo atoe ushahidi ndani ya siku 3.
Mwenyekiti
Andrew chenge amesema kuwa mbunge huyo alitakiwa kwa mujibu wa kanuni
za bunge kanuni ya 63(6) atoe ushahidi kwa ofisi ya bunge na ndani ya
siku zote ofisi ya bunge haijapata ushahidi huo.
Kutokana
na Mbunge huyo ambaye pia ni mke wa aliyekuwa mbunge wa Kigoma kusini
David Kafulila NCCR Mageuzi kushindwa kutekeleza maamuzi ya bunge
mwenyekiti wa bunge amemtaka kufuta kauli yake na mbunge huyo akakaidi
ndipo Mwenyekiti akamuamuru atoke nje mara moja na kutohudhuria vikao
vya bunge kwa siku zilizobakia 2.
Friday, February 5, 2016
CT-Scan Iliyopelekwa Muhimbili Ilikuwa Ya UDOM
WIZARA
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto imekiri kwamba
mashine ya CT Scan iliyofungwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
ilikuwa ni ya kituo cha kisasa cha kutolea huduma za afya cha Benjamin
Mkapa kilichopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Akijibu
swali la nyongeza bungeni mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Khamis Kigwangalla alisema
mashine hiyo iliingia nchini kwa lengo la kupelekwa katika kituo hicho
lakini ikapelekwa Muhimbili kutokana na kutokamilika kwa majengo ya
kufungwa mashine hiyo katika kituo hicho.
Alisema,
uamuzi huo waliuchukua pia kwa sababu hela ya kununua mashine nyingine
ambayo itapelekwa kufungwa katika kituo hicho ilikuwepo na kwa sasa
mchakato wa ununuzi unaendelea.
Dk
Kigwangalla alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Chemba, Juma
Nkamia (CCM) aliyetaka jibu la Serikali kama ni kweli ilichukua mashine
ya kituo hicho na kufunga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ama
ilinunua.
Awali
katika swali la msingi msingi, Nkamia alitaka kujua mpango wa Serikali
wa kununua mashine mpya ya CT -Scan kwa ajili ya Hospitali ya Taifa
Muhimbili.
Kuhusu
hilo, Dk Kigwangalla alisema, Desemba mwaka jana Serikali ilipeleka
mashine ya CT-Scan katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo
inatumia teknolojia ya kisasa yenye X-ray tube mbili na uwezo wa kupiga
picha ya 128 slice mara mbili.
Friday, February 5, 2016
Serikali Yajieleza Bungeni Kinachosababisha Umeme Ukatike Mara Kwa Mara
Serikali
imesema tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini linatokana na
uchakavu na kuzidiwa kwa vituo vya kupoza umeme na miundombinu ya
usafirishaji na usambazaji nishati hiyo.
Katika
kukabiliana na tatizo hilo Tanesco inachukua hatua za kujenga mifumo ya
njia kubwa za umeme wa msongo wa kilovoti 400 (Iringa-
Dodoma-Singida-Shinyanga), gridi ya Kaskazini Mashariki (Dar es Salaam,
Chalinze,Tanga –Arusha), ya Kaskazini Magharibi (Geita- Kagera –Katavi-
Kigoma- Rukwa na Mbeya) na Makambako- Songea wa kilovoti 220.
Kauli
hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk
Medard Kalemani wakati akijibu swali la Mbunge wa Magu, Boniventure
Kiswaga (CCM).
Kiswaga alitaka kufahamu serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo la kukatika katika kwa umeme.
Pia
mbunge huyo alitaka kufahamu, Je serikali itakamilisha lini kupeleka
umeme katika vijiji vya jimbo hilo ikizingatiwa mpaka sasa ni asilimia
20 tu ya vijiji ndiyo vina umeme.
Kalemani
akijibu swali hilo, alisema tatizo la kukatika kwa umeme linatokana na
uchakavu na kuzidiwa kwa miundombinu ya kupoza umeme pamoja na matukio
ya kulipuka kwa transfoma yanayosababishwa na radi hasa kipindi cha mvua
pamoja na wizi wa mafuta ya transfoma unaofanywa na wananchi wasio
waaminifu.
Alisema
Tanesco inakamilisha upanuzi wa usambazaji wa umeme katika majiji
makubwa ya Arusha, Dar es Salaam, na Mwanza ambapo kazi hizo zitahusisha
ujenzi wa njia mpya za umeme na kupanua vituo vya kupoza umeme.
“Kukamilika
kwa kituo cha kupoza umeme cha KIA mkoani Kilimanjaro kumeimarisha
upatikanaji wa umeme maeneo ya Mirerani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Kilimanjaro (KIA),” alisema Kalemani.
Pia
vituo vya kupoza umeme katika jiji la Dar es Salaam vya Gongo la Mboto,
Kipawa, Mbagala, na Kurasini vitaunganishwa kwa njia ya sakiti mzunguko
kutoka Ubungo na Kinyerezi kuanzia Machi mwaka huu.
Friday, February 5, 2016
Rais Magufuli Asema Yeye si Kichaa wala Dikteta......Aahidi Kuifanyia Mema Nchi hata Akifa awe Rais wa Malaika
RAIS
Dk. John Magufuli amesema anapochukua hatua yeye si kichaa, si dikteta,
si shetani wala si mnyama, ila ni mpole, lakini amefika mahali lazima
afanye hivyo kwani ndani ya Serikali yanafanyika mambo ya ajabu.
Kauli
hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam katika kilele cha Siku ya Sheria
nchini, alipokuwa mgeni rasmi kwa mara ya kwanza katika uzinduzi wa
Mwaka wa Mahakama tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Alisifu
kazi kubwa inayofanywa na Idara ya Mahakama, huku akitangaza uamuzi wa
gharama za kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge zaidi ya Sh
bilioni nne ni bora zikawasaidia wananchi.
“Ninapochukua
hatua mimi si mnyama, si dikteta, si shetani, ni mpole kweli, lakini
inafika mahali lazima nifanye, yanayofanyika serikalini ni mambo ya
ajabu sana, nataka kutoa sadaka yangu, inawezekana hata nikifa naweza
kuwa rais wa malaika,” alisema.
Alipongeza
kazi kubwa inayofanywa na mahakama huku akibaki kujiuliza kwanini
katika maadhimisho ya siku yao hawarushi matangazo yao moja kwa moja
kupitia luninga.
“Mnafanya
kazi kubwa, nilipofika niliuliza kwanini hii siku yenu hamrushi ‘live’,
nikajibiwa fedha za kurusha ‘live’ zinapelekwa kuwahudumia wananchi.
“Kipindi
kimoja kurusha ‘live’ kwa wiki mbili inatumika zaidi ya Sh bilioni nne,
ni vizuri kuzikata hizo fedha zinazopelekwa kurusha ‘live’ zikapelekwa
katika kesi za ubunge zinazohitaji shilingi bilioni tatu kusikilizwa
hadi kumalizika kwake,” alisema.
Alisema
mahakama ilikuwa inapewa bajeti ya Sh bilioni 41, lakini mwaka
2015/2016 ilishuka wakatakiwa kupewa Sh bilioni 12 ambazo hadi sasa
hawajapewa.
“Kiongozi
lazima ufikirie wapi pa kupeleka fedha na wapi pa kunyima, watu wa
mahakama mnafanya kazi ya Mungu, nawaahidi ndani ya siku tano nitakuwa
nimewapa Sh bilioni 12 zote.
“Sina
tatizo la masilahi ya wafanyakazi wa mahakama, katika bajeti ya mwaka
huu nitawapa fedha nyingi kuliko bajeti zote zilizopita, fedha zipo,” alisema.
Mahakimu Kutumbuliwa
Rais
Magufuli alisema anamwagiza Jaji Mkuu kuwachukulia hatua mahakimu 502
ambao hawakufikia malengo ya kumaliza kesi 250-260 kwa mwaka. Walimaliza
kesi chini ya 100.
“Mahakimu
ambao hawajafikia kumaliza kesi 260 hayo ndiyo majipu yako Jaji Mkuu,
unatakiwa kuyatumbua, wewe uliniapisha hata mimi, leo unapitisha agizo
mwingine anapinga.
“Unatoa
siku saba sasa sijui ndiyo watamaliza kutoa hizo hukumu, nakuagiza
wachukulie hatua, tusipochukua hatua hakuna kitakachofanyika.
“Walioshindwa
kufikia lengo unawabakiza wa nini, wasomi wako wengi, hata ukitangaza
leo watajitokeza, niruhusu mimi nitangaze, sitaki kuingilia mahakama,” alisema.
Mabilioni ya NIDA
Akizungumzia
hatua yake kwa watendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),
alisema ilipewa Sh bilioni 176.6, lakini vitambulisho vilivyotengenezwa
havifiki hata milioni mbili na havina sahihi wakati vitambulisho vya
kupigia kura fedha iliyotolewa haizidi Sh bilioni 70, lakini vina sahihi
za wapigakura wote wa Tanzania ambao ni milioni 23,253,982.
“Utaona
ugumu wa kuongoza, nchi inatawaliwa na madudu ya kila aina, wapo watu
wanacheza na fedha wanavyotaka wakati wapo watu masikini sana, wengine
wanataka bodi zao wakakae Ulaya.
“Hapo
ndipo tulipofikia, wengine wanalipwa mshahara kwa mwezi Sh milioni 35,
naomba mniombee kabla ya kunihukumu, toeni hukumu kwa haki kwa hawa
wanaotaka kuifikisha nchi pabaya, toeni hukumu zao haraka,” alisema.
Kesi za Wakwepa kodi
Rais
Magufuli alisema kuna kesi 442 za kukwepa kodi ambazo zingeamuliwa
Serikali ingepata Sh trilioni moja, ambayo ingeweza kununua ndege zaidi
ya sita.
Alimuomba
Jaji Mkuu kuzimaliza kesi 442 na kama zikimalizika fedha hizo Sh
trilioni moja ataipa Idara ya Mahakama Sh bilioni 259 na Sh bilioni 750
zilizobakia zitanunuliwa ndege sita na wafanyafakazi 250 ATCL waliopo
sasa wataondolewa.
Akizungumzia
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alisema kuna kesi 26 za watu
waliokutwa na nyara za Serikali, ambazo zipo zaidi ya miaka mitano
hazijaamuliwa kwa sababu upelelezi bado.
“Polisi
wapo, DPP yupo, upelelezi unaendelea kila siku, hapo unaona tatizo
lilipo, DPP upo unapeleleza nini au unatafuta rushwa?” alisema.
Alisema
suala la kuanzishwa kwa mahakama ya mafisadi ya wahujumu uchumi
halihitaji kwenda bungeni kufanya mabadiliko, lifanywe haraka, mahakama
ianze kwani nchi inachezewa.
Pamoja
na hali hiyo Rais Magufuli alikubali kupokea maombi yote yaliyotolewa
na mahakama na kuyazingatia kwani lazima ayaunge mkono ikiwamo kukubali
watumishi wa Idara ya Mahakama wasome na kupatiwa mikopo na Bodi ya
Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
“Nimeamua nchi iende na itaenda, anayefikiria ataikwamisha atakwama yeye, nategemea zaidi mahakama katika kufanikisha hilo,” alisema.
Subscribe to:
Posts (Atom)






























