Friday, March 4, 2016


Friday, March 4, 2016

Magufuli Asema Mafisadi Wakimshinda Asiitwe Rais



Rais Dk. John Magufuli amesema amejitolea kuwa sadaka kwa  Tanzania katika vita dhidi ya mafisadi na kwamba akishindwa kufanya hivyo, hakuna sababu ya yeye kuitwa rais.

Pia amesema wote waliotumbuliwa majipu watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Akizungumza jana katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika sehemu ya barabara ya Sakina hadi  Tengeru yenye urefu wa kilomita 14.1, itakayokuwa na njia nne, alisema ataendelea  kutumbua majipu kwa kuwa wanaonufaika na kudidimiza uchumi wa nchi ni wachache.

“Tumeanza kuchukua hatua ndogo ndogo, tunatumbua majipu. Mpaka sasa waliotumbuliwa si wengi kiasi hicho, hawajafika hata 2,000. Juzi juzi nimesikia baadhi ya watu wameanza kuwatetea wanaotumbuliwa, nasema hao wanaowatetea washindwe na walegee,” alisema.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi, Dk. Joseph Butore, Makamu wa Pili wa Rais wa Sudan Kusini, James Wani Igga, Balozi wa Japan nchini na mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Alisema wananchi wa Tanzania kwa muda mrefu wamekuwa wakipata shida na taabu kutokana na wachache kufilisi mali na rasilimali za nchi.

“Ifike mahali mmoja lazima ajitolee kufanya kazi hii. Mimi nimeamua kuwa sadaka kwa Tanzania, lazima tufanye kazi ya kutumbua majipu na kuwaletea maendeleo wananchi.

“Nisipofanya hivyo, hakuna sababu ya mimi kuitwa Rais. Hii  nasema kwa dhati kabisa kutoka moyoni mwangu, naomba Watanzania waniombee,”alisema.

Alisema kwa mfano yapo mambo ya hovyo ambayo hivi karibuni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeisababishia serikali upotevu wa fedha za matumizi ya simu nje ya nchi husika (roaming) kiasi cha Sh. bilioni 200.

Alisema watu wote wanaojihusisha na ufisadi watafukuzwa na kufikishwa mahakamani mwishowe kufungwa ili nao wakapate machungu.

“Hii nchi ilifika mahali ikawa kama  shamba la bibi vile,” alisema na kusisitiza kuwa katika kuwaletea wananchi maendeleo hatafanya ubaguzi wowote kwa kuzingatia vyama, dini, kabila ila atachapa kazi tu.

“Nawaomba Arusha tujenge umoja wetu, tusibaguane. Tukianza kujenga umoja wa Tanzania na tukaunganishaa na umoja wa Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini, Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa na maendeleo ya kasi," alisema Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Aliongeza kuwa: "Tukiamua tunaweza kubadilika na kuwaletea wananchi wa jumuiya hii maendeleo makubwa.”
 
Alisema wananchi wa EAC wanachohitaji si vyama ila kazi, maendeleo na maisha mazuri na si kuwafanya wachache wawe wanafaidi kuliko wengine.

Awali, alimpongeza Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), kwamba ni mtu mchapakazi.

“Nampongeza sana Nassari, ni kijana safi anachotaka ni kazi na ameweza kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo lake.

"Sipendi kuwa mnafiki, nampongeza sana Nassari. Ukimtazama usoni Nassari ni Chadema lakini kwa kweli moyo wake uko CCM,” alisema na kufanya umati wa watu kulipuka kwa shangwe.

Mapema Rais Museveni alisema: “Tukiwa tunazungumzia uchumi wa kisasa, Afrika hakuna umaskini, ina utajiri mwingi wa raslimali isipokuwa inakosa maendeleo tu.

“Ardhi ipo, madini yapo, lakini tunashindwa kuzitumia, hivyo tunakosa maendeleo, tunakosa elimu na tuna afya duni,” alisema.

Aliwataka wananchi kujikita katika kilimo cha kisasa badala ya kulimia tumbo peke yake.

Museveni alisema sekta ya kilimo, viwanda, huduma na ICT, ndizo zinazoweza kuleta maendeleo kwa nchi za EAC.

Hata hivyo, alisema shida ya Waafrika ni kulala na kwamba wanalala huku kukiwa kumekucha na kusisitiza kuwa: 
 
“Tukiamka sisi sote tutakuwa na maendeleo kutokana na uzalishaji mkubwa utakaokuwapo," alisema.

Aliwaondoa wananchi hofu ya kupatikana kwa soko pale aliposema jumuiya hiyo ina watu zaidi ya milioni 160, hivyo idadi hiyo ni soko kubwa kwa bidhaa zitakazokuwa zikizalishwa na wananchi.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta, alisema, viongozi wa jumuiya hiyo ndio waliofanya kazi ya kulala wakati kumekucha.
Alisema kazi kubwa waliyonayo wao ni kuwaletea maendeleo wananchi kwa kujenga miundombinu.

Aliwataka viongozi wenzake kubadilika badala ya kuwa na maneno mengi na kwamba sasa wawe watu wa kazi ambayo itawawezesha wananchi kupata maendeleo na kuyafurahia.
==

Friday, March 4, 2016

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini Arejeshwa Nchini


Balozi  Radhia Msuya
Rais Dk. John Magufuli, amemrudisha nyumbani aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya, pamoja na watumishi wengine watano, baada ya muda wao kumalizika.

Hii ni mara ya pili kwa Rais Dk. Magufuli kuwarejesha nyumbani Mabalozi wa Tanzania walioko nchi za nje baada ya muda wao wa mkataba kumalizika.

Ikumbukwe kuwa Januari 25, mwaka huu, Rais Magufuli alimrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Peter Kallaghe, kuja kufanya kazi Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Dk. James Msekela na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Japan, Dk. Batilda Buriani, baada ya mikataba yao kumalizika.

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, amesema kurudhishwa nyumbani kwa Balozi Msuya, ni jambo la kawaida kwa sababu bado kazi ya kuwarudisha nyumbani Mabalozi waliomaliza mikataba yao linaendelea.

Alisema kwa sasa serikali inachofanya ni kuwarudisha nyumbani Mabalozi ambao mikataba yao imemalizika na kuwapeleka watumishi wengine wakapate uzoefu nje ya nchi.

Alisema kuna makundi matatu ambapo kundi la kwanza ni watumishi wa idara ambao muda wao wa miaka mitano umemalizika ambao wanarudishwa nyumbani ama kuhamishiwa kituo kingine cha kazi.

Alisema kundi la pili ni la Mabalozi ambao siyo watumishi wa wizara, lakini waliteuliwa na Rais kwa mkataba, hivyo mikataba yao ikimalizika Rais mwenyewe ndiye anayeamua kama ni kuwaongezea au kusitisha na kurudi nyumbani.

Dk. Mahiga alitaja kundi la tatu kuwa ni Mabalozi ambao muda wao wa kukaa nje umemalizika au umri wao wa kustaafu umefika, lakini mikataba yao bado haijamalizika, hivyo Rais anaamua kuwarudisha nchini ili wapumzike na wengine wakashike nafasi zao.

Alisema kuna Mabalozi ambao mikataba yao ya kufanya kazi nje ya nchi ni miaka mitano, lakini wamekaa zaidi ya miaka 10, hivyo serikali iko katika mchakato wa kuwarudisha nyumbani.

Waziri Mahiga alisema kuna vituo zaidi ya 35 ambavyo vinatakiwa kuwa na Mabalozi, hivyo serikali itahakikisha inawarudisha nyumbani mabalozi waliomaliza muda wao wa kazi na kupangiwa majukumu mengine.
==
Friday, March 4, 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Akabidhiwa zana ya ‘Kisukuma’ Kukabili MAJIPU......Pia Kapewa Jina Jipya ambalo ni Masanja Mkusanyaji



WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepewa jina jipya la Kisukuma na kukabidhiwa zana nyingine muhimu katika vita ya kupambana na ufisadi nchini maarufu kwa jina la kutumbua majipu.

Kuanzia juzi, Waziri Mkuu Majaliwa atakuwa akifahamika kwa jina lingine la Masanja, alilopewa na Wazee wa Kisukuma wa Lamadi wilayani Busega katika mkoa wa Simiyu. 
Kabla ya kuwahutubia maelfu ya wakazi wa Lamadi juzi jioni, wazee hao walimvisha Waziri Mkuu vazi la kijadi la Kisukuma akiwa katika kigoda, wakamkabidhi usinga, ng’ombe wawili na mkuki ambao walimueleza kuwa kazi yake ni kuendeleza vita ya ufisadi kwa kuutumia kutumbua majipu.

“Tunakukabidhi usinga na huu mkuki utumike kutumbua majipu kwa sababu kazi hii unaifanya vizuri hadi sasa, kwa hiyo uendelee kutumbua majipu. Na kwa kuanzia sasa, tunakupa jina la kwetu, kwa sababu wewe ni kijana wetu, utaitwa Masanja,” alisema Mchele Malale kwa niaba ya wazee wenzake.

Kwa mujibu wa wenyeji, jina la Masanja lina maana ya kuingia kokote, hali inayomaanisha kuwa Waziri Mkuu Majaliwa aendelee kutumbua majipu kila mahali.
Alipoanza kuhutubia, Waziri Mkuu alikiri kuwa amepata mapokezi makubwa kwa wananchi wa Lamadi, na zaidi, makubwa kuliko sehemu nyingi alizokwenda tangu ashike wadhifa wake huo.

“Kwa kweli nimefurahishwa na mapokezi yenu hapa…tangu nilipotoka Mwanza hadi kufika kwenu (Busega) mapokezi yamekuwa mazuri, na hapa Lamadi mmetisha. Mmenitia faraja sana,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza: 
“Lakini nimefurahi kwa zawadi mlizonipa na pia jina jipya la Masanja.Nimeandika pale kwenye diary (shajala) yangu. Mmenipa pia mkuki, mmesema nitumie kama sindano kuendeleza ile kazi,” alisema Waziri Mkuu na kushangiliwa na maelfu ya wakazi wa Lamadi.

Akiwa Bariadi jana, Waziri Mkuu alisema jina lake sasa ni Masanja Mkusanyaji, na kwamba ataendelea kukabiliana na wakwepa kodi na mafisadi ili Watanzania wapate huduma stahiki.
==

Tuesday, March 1, 2016


Wednesday, March 2, 2016

Polisi ,UKAWA Ngoma Nzito........Naibu Katibu Mkuu CUF Nassor Ahmed Mazrui Naye Atakiwa 'Kujisalimisha' Polisi Kwa Mahojiano



Jeshi la Polisi limeendelea na kamatakamata ya wapinzani wa vyama vinavyounda Ukawa katika maeneo mbalimbali likieleza sababu tofauti za kijinai zinazohusishwa na masuala ya kisiasa.

Mpaka sasa wabunge wa upinzani waliokamatwa ni; Halima Mdee (Kawe), Mwita Waitara (Ukonga) na Peter Lijualikali (Kilombero), wote wa Chadema na baadhi ya madiwani wa chama hicho katika Jiji la Dar es Salaam.
Vilevile, imeelezwa kuwa Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alikuwa anatafutwa kuunguanishwa na wenzake.

Pia, baadhi ya wanasiasa wa CUF Zanzibar wamekamatwa na kuhojiwa kwa madai ya kuwatusi viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ). 
Viongozi wa CUF waliohojiwa na polisi mpaka sasa ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Omar Ali Shehe na Kiongozi wa Mkakati wa Ushindi, Mohamed Sultan Mugheir ‘Eddy Riyami’ ambaye yuko nje kwa dhamana.  

Mbali na viongozi hao, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui  jana  amepatiwa barua ya wito  na Polisi Zanzibar  ikielezwa kuna mambo yanamhusu.

Hii ni mara ya pili kwa Mazrui kuitwa polisi tangu kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25, huku CUF ikidai kuwa huo ni mwendelezo wa mkakati maalumu dhidi ya viongozi wa chama hicho.
Jana, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Umma wa CUF, Maalim Hamad Masoud Hamad alidai kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya kisiasa ya kutaka kumkamata kila kiongozi wa juu wa CUF kuelekea uchaguzi wa marudio.

“Kwa viongozi wa CUF hili halishangazi, nahisi ingelikuwa ni hatua ya kushangaza sana iwapo wanaoitwa kuhojiwa na polisi ni viongozi wa vyama vingine.

"Sisi upande wetu hili ni jambo la kawaida mno na watu wasishangae,” alisema.

Mazrui ambaye pia alikuwa Waziri wa Biashara na Uwekezaji, ametakiwa kuripoti Makao Makuu ya Polisi, Ofisi ya Upelelezi Ziwani mjini hapa kesho saa 2.00 asubuhi na kuonana na mkurugenzi wa makosa ya jinai Zanzibar.

Polisi Zanzibar imethibitisha kuwapo wito huo ikisema kuna mambo muhimu yanayomhusu mwanasiasa huyo.