Tuesday, February 23, 2016

Lipumba Amtaka Rais Magufuli Atangaze Mshahara Na Marupurupu Yake



Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka Rais John Magufuli atangaze mshahara na marupurupu yake, kwa kuwa amejivisha joho la kuwa Rais wa wanyonge.

Profesa Lipumba amelieleza gazeti la Mwananchi kuwa Rais Magufuli amejipambanua kuwa kiongozi anayeguswa na matatizo ya wanyonge, hapendi makuu, anahimiza ukusanyaji wa mapato ya Serikali na matumizi mazuri ya fedha za umma, lakini watanzania hawajui mshahara wake ni kiasi gani

Profesa huyo aliyejikita katika masuala ya uchumi, alirejea mijadala mbalimbali iliyowahi kuibuliwa kuhusu mshahara wa Rais, ikiwamo ule uliyowahi kuibuliwa mwaka 2013 na Zitto Kabwe, wakati huo akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema kuwa Rais analipwa Sh32 milioni kwa mwezi.

Pia alirejea taarifa iliyochapishwa na Mwananchi, Julai 27, 2015, iliyoandikwa kutoka katika mtandao wa African Review kuwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete ni wa nne miongoni mwa marais wa Afrika kwa kupata mshahara mkubwa wa dola za Marekani 192,000 kwa mwaka sawa na dola 16,000 kwa mwezi, ambayo ni sawa na Sh32 milioni kwa mwezi. Hadi jana jioni, dola moja ya Marekani ilikuwa sawa na Sh2,187.

“Taarifa ya Ikulu ilikanusha vikali habari zilizochapishwa na Mwananchi. Ikulu ilieleza kuwa habari hizo siyo za kweli. Hata hivyo, haikueleza mshahara wa Rais na marupurupu yake ni kiasi gani?

Pia, katika mjadala wa mshahara wa Rais, Naibu Spika wa Bunge lililopita ambaye ndiye Spika wa sasa, Job Ndugai alinukuliwa akieleza kuwa mshahara wa mtu ni siri yake.

Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma wa wakati huo, Celina Kombani (kwa sasa ni marehemu) alisema kuwa ni kosa kutangaza mshahara wa Rais.

“…Kwa hivi sasa Rais Magufuli atangaze mshahara na marupurupu yake na kama mapato yake ni Sh32 milioni kwa mwezi, basi ajitolee alau nusu ya mapato hayo kuchangia elimu na afya ya wanyonge. Hatua hii itaimarisha taswira inayojengeka barani Afrika kuwa yeye ni Rais wa wanyonge,” amesema  Lipumba.

Wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam wiki iliyopita, Rais Magufuli aliwataka mawaziri, naibu mawaziri na makatibu wakuu wachangie Sh1 milioni katika mishahara yao kuchangia elimu.

Pia Rais alieleza kuwa yeye mwenyewe, makamu wake na waziri mkuu watachangia Sh6 milioni kila mmoja, ili zifike Sh100 milioni kusaidia changamoto za elimu bure Mkoa wa Dar es Salaam.

Kutokana na tangazo hilo, Profesa Lipumba alisema, “Ikiwa Sh6 milioni zitakatwa katika mshahara wake wa mwezi mmoja ni wazi mshahara wake na ule wa makamu wake na waziri mkuu ni zaidi ya Sh6 milioni kwa mwezi.

“Mishahara na marupurupu ya viongozi wa Tanzania hayako wazi. Watanzania hawajui kila mwezi Rais, Makamu wa Rais na viongozi wakuu wa Serikali wanalipwa kiasi gani? Malipo ya wabunge pia hayako wazi?” alihoji.

Profesa Lipumba ambaye amewahi kuwa msaidizi wa Rais katika masuala ya uchumi kati ya mwaka 1991 na 1993, alisema kwa kuwa Rais Magufuli amejivisha joho la kuwa Rais wa wanyonge, anawajibika kuwaeleza Watanzania mshahara na marupurupu yake.

“Ikiwa mshahara ni mkubwa sana achukue hatua za kuupunguza kama alivyofanya Mwalimu Nyerere mwaka 1965.”

Hata hivyo, alisema kifungu cha Katiba cha 43 (2) kinaeleza kuwa mshahara na malipo mengineyo yote ya Rais havitapunguzwa wakati Rais atakapokuwa bado ameshika madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba.

Profesa Lipumba alisema Rais Magufuli akitaka kupunguza mshahara wake itabidi kwanza abadilishe kifungu hicho cha Katiba.

“Anaweza kujitolea mchango wa kudumu utakaokatwa kutoka kwenye mshahara wake kusaidia sekta ya afya au elimu,”alisema.

Profesa Lipumba ambaye ni mshauri wa Benki ya Dunia (WB) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika masuala ya uchumi, alisema ili kuimarisha utawala bora ni muhimu uongozi ulio madarakani utumie mamlaka waliopewa kwa manufaa ya Taifa.

“Mishahara na marupurupu ya viongozi yawe wazi na yaamuliwe na kupangwa na taasisi iliyo huru. Kuweka utaratibu ulio wazi wa kuamua mishahara na marupurupu ya viongozi wa umma wakiwamo Rais na makamu wake, mawaziri, wabunge, majaji, makatibu wakuu na viongozi wengine,”alisema.

Alisema ni muhimu katika ujenzi wa utawala bora, uwajibikaji na uwazi wa viongozi wa umma kwa wananchi wanao waongoza.

“ Inasemekana mshahara wa mbunge katika Bunge lililopita ulikuwa Sh3.4 milioni kila mwezi.Pia mbunge alilipwa Sh8.2 milioni, nyingine kama posho ya jimbo, gharama za ofisi, mafuta, malipo ya wasaidizi wake na dereva.

“Vile Vile, mbunge anapohudhuria kikao cha Bunge alilipwa posho ya Sh80,000 za kujikimu, Sh50,000 za mafuta ya gari na Sh200,00 za kuhudhuria kikao cha Bunge, jumla ni Sh330,000 kwa siku.

“Posho ya siku moja ya mbunge ni zaidi ya mara mbili ya kima cha chini cha mshahara wa Serikali kwa mwezi mzima ambacho ni Sh150,000. Mishahara inakatwa kodi, marupurupu hayakatwi kodi,”alisema.

Magufuli Atinga GHAFLA Kivukoni na Magari yenye Namba za Kawaida



Rais John Magufuli ameendelea kufanya ziara za kushtukiza, baada ya kutembelea ofisi za Kivukoni Dar es Salaam kimyakimya juzi jioni kuangalia mwenendo wa utoaji huduma za vivuko.

Mashuhuda waliokuwepo eneo hilo Jumapili jioni wakati Rais anafanya ziara hiyo, walieleza mtindo alioingia nao Dk Magufuli ulikuwa ni wa kawaida na vigumu kwa mwananchi wa kawaida kung’amu uwapo wa Rais.

Mfanyabiashara wa eneo hilo, Sharif Mkamba alisema Rais Magufuli aliingia saa 11 jioni akiwa na msafara wa magari matatu ya kawaida yaliyokuwa na namba za kiraia.

“Hakukuwa na king’ora chochote kama tulivyozoea bali ulikuwa ni msafara wa kimya kimya. Aliingia moja kwa moja kwenye zile ofisi na alitumia kati ya dakika 10 hadi 15 kabla ya kutoka,” alisema Mkamba.

Said Likoko alisema kuwa baada ya kugundua kati ya magari matatu alikuwepo Rais, walisogea kufuatilia kwa kina kwa kuwa haijazoeleka na walitegemea huenda baadhi ya watumishi wangewajibishwa.

“Aliteremka na kumuuliza aliyemkusudia na taarifa tulizozipata jana zinadai hakumkuta huyo bosi, sijui ni meneja au ofisa sisi hatujui,” alisema Likoko ambaye hujishughulisha pia na biashara ndogondogo eneo la kivukoni.

Likoko alisema pamoja na kwamba aliingia kimya kimya, Rais Magufuli hakusita kuwasalimia wasafiri waliokuwa wakisubiri kivuko wakati alipofanya ziara hiyo.

Alieleza kuwa kama wananchi walifurahishwa na hatua hiyo ya Rais, kwa kuwa watendaji wengi hawafanyi kazi siku za wikiendi licha ya huduma zake kufanyika siku zote.

Tangu jana asubuhi kumekuwa na video inayosambaa ikimuonyesha Rais Magufuli akiwa Kivukoni akitembea kwa miguu ndani ya eneo hilo huku akishangiliwa na wasafiri waliokuwa wakingoja kivuko.

Hata hivyo, jitihada za kutafuta mamlaka husika kueleza kwa undani malengo ya ziara hiyo ziligonga mwamba baada ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kutopokea simu.

Ofisa habari wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) Theresia Mwami, alitaka utafutwe uongozi wa juu kueleza yaliyojiri kwenye ziara hiyo kwa kuwa yeye yupo likizo.

Tuesday, February 23, 2016

Rais Mugabe Atimiza miaka 92.....Wasaidizi wake Wasema Atawania Tena Urais Mwaka 2018



Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ametimiza umri wa miaka 92 huku chama chake kikisema atawania tena urais 2018.

Mnadhimu wake mkuu alisema kiongozi huyo ambaye ameongoza nchi tangu mwaka 1980, bado ana uwezo kamili wa kuongoza Serikali licha ya tetesi kwamba hawezi kuongoza kutokana na umri.

Akizungumza na gazeti la Serikali Sunday Mail, Katibu Mkuu wa Rais Misheck Sibanda alisema tetesi hizo si za kweli na hazina msingi kwani Mugabe ana ratiba ya wiki nzima kutekeleza kazi za Serikali na chama.
Rais Mugabe ambaye aliapa kuongoza nchi hadi atakapokufa, alishinda kipindi kingine cha urais cha miaka mitano kwenye uchaguzi wa mwaka 2013 uliofanyika chini ya katiba mpya inayoweka ukomo wa kuongoza kwa vipindi viwili tu vya miaka mitano.

Chama chake tayari kimetangaza kumpitisha Mugabe kama mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2018.

Mugabe amekua kiongozi wa Zimbabwe tangu 1980. Ni mwenyekiti wa chama tawala cha Zanu. 1980 alikuwa waziri mkuu na 1987 Rais wa Zimbabwe.

Utawala wa Mugabe umeitwa wa kidikteta tangu mwaka 2002 kutokana na  kudharau haki za binadamu nchi Zimbabwe.

Uingereza Yammwagia Sifa Rais Magufuli Kwa Kasi Yake Ya Kukusanya Mapato na Kupambana Na Wala Rushwa



Nchi ya Uingereza imempongeza Rais John Magufuli kwa utendaji wa serikali yake hususani katika kupambana na ubadhirifu wa mali za umma na ufisadi, kwa siku chache alizokaa madarakani.

Sifa hizo za Uingereza zimewasilishwa jana Ikulu jijini Dar es Salaam na Balozi wa nchi hiyo,, Balozi Dianna Melrose.

Balozi Melrose alieleza kuwa nchi yake imeridhishwa na juhudu za Rais Magufuli katika kulinda fedha za umma na kuahidi kushirikiana naye hususan katika kuimarisha idara ya Mahakama na Intelijensia nchini.

“Tunadhani ameonesha msimamo mkali dhidi ya rushwa na ufisadi, na miongoni mwa mambo ambayo tumezungumza ni namna ya kufanya kazi pamoja katika kupambana na rushwa. Tuna mazungumzo katika kuimarisha mifumo ya kiintelijensia na mahakama,” alisema Balozi Melrose.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alikutana na rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete Ikulu lakini mazumgumzo kati yao hayakuwekwa wazi.

Monday, February 22, 2016

Rais Magufuli Kuwatema Wakuu wa Mikoa 20



Wakati  Rais Dk. John Magufuli akitarajia kutangaza safu ya wakuu wa mikoa  na wilaya wapya, imebainika wapo zaidi ya 20 ambao watatemwa kutokana na sababu mbalimbali za utendaji.

Habari za kuaminika zinasema miongoni mwa  wakuu wa mikoa watakaoachwa wamo walioshindwa kutatua kero sugu zikiwamo za mapigano ya wakulima na migogoro ya ardhi ambayo kila kukicha imesababisha watu kadhaa kufariki dunia.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, pia wamo wakuu wa mikoa  ambao wanaweza kuachwa kutokana na kuwa na umri mkubwa na wanaonyesha wazi hawawezi kwendana na kasi ya utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano ambayo inatumia falsafa ya Hapa Kazi Tu.

Habari hizo zinasema wapo wakuu wa mikoa ambao wameshindwa kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao kwa zaidi ya miaka 10 hadi 15 na kusababisha vurugu kuibuka kila wakati.Miongoni mwa mikoa iliyokithiri kwa migogoro hiyo ni Morogoro, Tanga na Manyara.

“Wapo wakuu wa mikoa  ambao hawatarudi kutokana na rekodi za matukio, wapo ambao kwenye maeneo yao   migogoro imedumu kwa zaidi ya miaka 10 na kuendelea, sasa viongozi wa aina hii unadhani watabaki kweli kwenye Serikali?

“Nakuhakikisha kule ambako kuna migogoro ya ardhi na mapigano ya kila siku wako hatarini kupoteza kibarua… unajua mheshimiwa kila siku anajiuliza hivi inakuwaje mkoa ambao una kamati za ulinzi na usalama za wilaya zinashindwa kuchukua hatua za kumaliza mapigano haya?

“Inawezekana zinafanya kazi kwa kutegeana au wengine wanakula kwa wafugaji na wakulima.

“Mpaka wiki iliyopita tumedokezwa kwamba ma-RC  20 hawatarudi katika nafasi zao kwa sababu wameshindwa kuonyesha kama wanaweza kuwajibika ipasavyo,” kilisema chanzo cha habari hii.

Chanzo  hicho kilisema pia kuwa wengine ambao wako hatarini kutemwa ni wale wenye umri mkubwa ambao kwa namna moja au nyingine wanapaswa kustaafu.

“Sikutajii ni mikoa gani kwa sababu hawa wanajulikana vizuri…pale kanda ya ziwa, nyanda za juu kusini na mikoa ya kaskazini ni maeneo  ambayo yataguswa mno.

“Unajua Dk. Magufuli na timu yake wanaangalia kwa kina mno  hata mikoa ya kanda ya magharibi nao hawako salama kwa sababu wapo wazee wetu ambao inaonekana wazi umefika wakati wa kupisha kizazi kingine ambacho kitasaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo,”kilisema chanzo chetu.

Kuhusu wakuu wa wilaya, chanzo hicho kilisema hakuna tofauti na wakuu wa mikoa kwa vile kila mmoja atapimwa kutokana na namna alivyoweza kusimamia majukumu ya Serikali tangu alipoteuliwa.

“Jambo moja kubwa ndugu yangu, hapa kila mmoja atapimwa kutokana na uwezo wake… nadhani unakumbua Rais mwenyewe alisema anawachunguza, tutarajie mabadiliko makubwa,” kilisema chanzo chetu.

Hivi karibu Rais Magufuli, alisema wakuu wa mikoa na wilaya wajiandae kuwajibika endapo maeneo wanayoongoza yatakuwa na ukosefu wa chakula na kusababisha wananchi kukumbwa na njaa wakati maeneo mengi ya nchi yamepata mvua ya kutosha.

Mikoa ambayo imekuwa ikikumbwa   na njaa mara kwa mara  ni pamoja na Mara, Iringa, Dodoma,Tanga na Shinyanga.

Mpinzani wa Museveni, Dr. Besigye Akamatwa Tena........Museven Aeleza Sababu za Kumpa Kifungo Cha Nyumbani



Kiongozi wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC) nchini Uganda Kizza Besigye amekamatwa tena na maafisa wa polisi. Dr. Besigye amekamatwa alipokuwa akijaribu kuondoka nyumbani kwake.
 
Rais Yoweri Museveni  leo asubuhi  aliongea  na  BBC na kusema kuwa  serikali yake iliamua kumpa kifungo cha nyumbani  ili kuzuia vurugu baada ya zoezi la kupiga kura na kutangaza matokeo.

Museveni alieleza kuwa walichukua uamuzi huo baada ya kubaini kuwa Dk. Besigye alipanga kutangaza matokeo yake mwenyewe ambayo sio ya kweli na kuhamasisha wafuasi wake kufanya fujo, vitendo ambavyo havikubaliki.

“Walikuwa wanataka kufanya fujo. Kwanza walikuwa wanataka kutangaza matokeo yao wenyewe ya uongo. Pili walitaka kufanya fujo za kuharibu mali,” alisema Museveni.

Kadhalika, Museveni alieleza kuwa serikali yake haina mpango wa kuweka ukomo wa Urais nchini humo kwakuwa tayari Bunge liliona ni vyema kuwa na kipindi kisichokuwa na ukomo. Hata hivyo, alisema kuwa hana mpango wa kufanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo ili aendelee kubakia madarakani.

“Hakuna mpango wowote. Hatujazungumzia hilo. Lilikuja kwenye baraza la mawaziri tukasema hapana, hakuna haja ya kuongeza,”Museveni anakaririwa.
Katika hatua nyingine, Museveni ambaye anaiongoza Uganda tangu mwaka 1986, amepinga ripoti za waangalizi zilizodai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na haki.

Alisema kuwa wanaotoa madai hayo kwa madai kuwa nguvu ya jeshi ilitumika zaidi hawaijui siasa ya Uganda kwani wanasiasa wengi hawajakomaa kisiasa hivyo wanaweza kuanzisha fujo muda wowote.

Monday, February 22, 2016

Majipu Yaendelea Kutumbuliwa......Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Asimamishwa Kazi



WAZIRI  wa nchi,ofisi ya Rais menejimenti ya utumishi  wa Umma na Utawala bora,Angella Kairuki amemsimisha kazi mkuu wa chuo cha utumishi wa umma nchini Said Nassoro kutoka na uzembe ulioisababishia serikali  hasara  ya  bilioni 1.
 
Vilevile Waziri Kairuki amewasimamisha  kazi Mkuu wa chuo hicho tawi la Dar es salaam,Joseph  Mbwilo na Silvanus  Ngata ambaye naye ni Mkuu wa chuo hicho tawi la Tabora.
 
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam,Waziri Kairuki amesema amefikia hatua hiyo ya kuwasimamisha kazi watumishi hao baada ya kubaini utendaji usioridhisha katika vyuo hivyo.
 
Amesema Nassoro amemsimisha kazi baada ya kushindwa kuwasimamia watumishi wa chini yake katika  chuo hicho.
 
“Mwaka  2011 hadi  2013 bwana Silvanus Ngata aliongeza gharama za ujenzi wa jengo la chuo hicho tawi la  Mtwara tofauti na fedha iliyokuwa imepangwa.  

"Chakushangaza, huyu Nassoro ambaye ni mkuu wao,  baada ya kugundua kosa hilo alishindwa kumuwajibisha na badala yake aliamua kumhamishia tawi la chuo cha Tabora. Sasa mimi nawasimamisha kazi wote ."Amesema Kairuki
 
Pia waziri Kairuki amesema amemsimamisha Mbwiro kutokana na matumizi mabaya ya fedha za chuo.
 
“Huyu Mbwiro kwa mwaka 2013 alitumia vibaya fedha za ada za wanafunzi  kiasi cha bilioni 1 ,lakini licha ya ubadhilifu huo, Nassoro alimteua bwana Mbwiro kuwa Kaimu mkuu wa chuo kwa upande wa fedha." Alisema Waziri Kairuki.
 
Wakati Waziri Kairuki akitumbua majipu hayo,mmoja wa watendaji hao,Said Nassoro alikuwepo kwenye mkutano huo na wanahabari huku akiwa hajui kinatakachotokea